top of page
Search
  • Martin Mponzi

Martin Gabriel Mponzi - Kijana na Afya Bora YAI Fellow

Updated: 3 days ago



Safari Yangu ya Kujifunza na Kukuza Uongozi

Nakumbuka vizuri ile siku nilipoomba kufanya kazi na Young & Alive (YAI). Haikuwa kazi rahisi kuomba nafasi hiyo ya mafunzo ya mradi huu wa Kijana na Afya Bora, lakini moyo wangu ulikuwa na matumaini makubwa. Ilipofika siku ya kujibiwa, nilipokea ujumbe mzuri kwamba nimechaguliwa kujiunga na timu. Furaha niliyopata siku hiyo haiwezi kuelezeka kwa maneno! Kwangu ilikuwa ni hatua kubwa katika safari yangu ya kujifunza na kujenga ujuzi wangu katika masuala ya uongozi na afya ya uzazi.


Baada ya kuchaguliwa, tulianza mafunzo yetu kwa njia ya ZOOM (online), ambapo tulipata fursa ya kujifunza mambo mengi mapya. Miongoni mwa yale ambayo nilijifunza ni:

  • Uongozi katika ngazi tofauti: Hapa nilielewa umuhimu wa kuwa na uongozi wenye ngazi tofauti na jinsi ngazi hizi zinavyosaidia kufanikisha malengo ya pamoja.

  • Umuhimu wa ngazi mbalimbali katika uongozi: Tulijifunza jinsi kila ngazi inavyochangia kufanikisha uongozi mzuri.

  • Kujitambua kama kiongozi: Tuligusia sana jinsi kiongozi anapaswa kujifahamu, kujua majukumu yake, na kuelewa ni nini kinachomfanya kuwa kiongozi bora.

  • Sifa za kiongozi bora: Nilipata nafasi ya kujifunza sifa ambazo kiongozi anapaswa kuwa nazo ili aweze kuongoza kwa ufanisi.

  • Namna ya kuishi na jamii: Tulijifunza umuhimu wa kuishi vyema na jamii ili kuwa kiongozi anayekubalika na kuheshimika.


Haya ni baadhi tu ya masomo mengi niliyojifunza. Mafunzo haya ya mradi huu wa Kijana na Afya Bora yalikuwa na maana kubwa katika safari yangu ya uongozi, na yamenifanya niwe na mtazamo mpana zaidi juu ya uongozi na namna ya kushirikiana na jamii.


Maboresho Katika Mafunzo

Pamoja na mafanikio ya mafunzo ya mradi huu wa Kijana na Afya Bora, ningependa kupendekeza maboresho kadhaa kwa siku zijazo.

  • Kwanza, ni muhimu tujitahidi kwenda na ratiba kwa wakati, kwani katika kipindi hiki tulikuwa na changamoto ya kuahirisha baadhi ya vipindi.

  • Pili, napendekeza mafunzo yawe yanafanyika ana kwa ana badala ya mtandaoni. Nafikiri kwamba mafunzo ya uso kwa uso yanaweza kumsaidia mtu kuelewa vizuri zaidi kuliko mafunzo ya mbali.


Uzoefu Wangu Katika Fieldwork

Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kutengeneza mahusiano mazuri na jamii ya Kituo cha Afya Lupalilo na Zahanati ya Mago. Ushirikiano nilioupata kutoka kwa wahudumu wa vituo vya afya na zahanati ulikuwa wa hali ya juu. Tuliweza kufanya kazi kwa pamoja kwa amani na kuelewana vizuri, jambo ambalo lilirahisisha utekelezaji wa majukumu yetu.


Pia, kupitia mafunzo ya mradi huu wa Kijana na Afya Bora imenijengea mahusiano mazuri na wanakijiji wa maeneo yangu. Sisi kama vijana tulikaa pamoja na kujadili masuala ya uzazi wa mpango kwa ujumla, na vijana walitupatia ushirikiano mzuri sana. Katika Zahanati ya Mago na Kituo cha Afya Lupalilo, huduma za afya ya uzazi kwa vijana zinapatikana, ingawa kuna changamoto ndogo kwa wapokeaji wenyewe. Vijana wengi hawapati huduma hizi mara kwa mara kama inavyopaswa. Tulihimizana sisi kama vijana kuwa na utamaduni wa kwenda vituoni mara wanapohitaji huduma za afya ya uzazi, kwani huduma hizi zinapatikana kwa wingi.


Safari yangu na Young & Alive kupitia mafunzo ya mradi huu wa Kijana na Afya Bora umekuwa wa manufaa makubwa kwangu. Nimepata ujuzi mwingi na kujenga uhusiano na jamii, jambo ambalo limenifanya niwe na hamasa zaidi ya kuendelea kutumikia jamii na vijana kwa ujumla.

13 views0 comments

Comments


bottom of page