top of page
Search
  • Eunice Herman Joseph

Eunice Herman Joseph - Kijana na Afya Bora, YAI Fellow, Mbeya.



Safari Yangu Kama Champion Katika Mradi wa Kijana na Afya Bora

Naitwa Eunice Herman Joseph, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika kada ya Ufamasia, na pia ni Champion katika mradi wa Kijana na Afya Bora unaoendeshwa na Young & Alive Initiative. Nilipoanza safari yangu na mradi huu wa Kijana na Afya Bora, niliweka lengo la kujifunza kitu kipya, na ukweli ni kwamba, niliweza kupata maarifa mengi sana kupitia mafunzo niliyopitia. Nimejifunza kuhusu uongozi, upatikanaji wa huduma za afya katika jamii, haswa kwenye ngazi ya vituo vya afya.


Mafunzo na Uongozi

Katika mafunzo haya kupitia mradi huu wa Kijana na Afya Bora, nimepata fursa ya kujifunza aina mbalimbali za uongozi, namna ya kuongoza watu na hata jinsi ya kuwa kiongozi mzuri katika maisha yangu binafsi. Uzoefu huu umenisaidia sana kuongeza ujasiri na kujiamini, hususan wakati wa kutekeleza mradi wetu. Ningependekeza pia kuwe na mazingira mazuri ya kuwajenga Champions kwa pamoja, kama vile kuunda magrupu ya kujadili na kubadilishana mawazo ili kuongeza ujasiri na kujenga ushirikiano mzuri.


Uhusiano na Jamii

Uhusiano wangu na jamii katika masuala ya afya ni mzuri kutokana na kada yangu ya ufamasia. Nimeweza kuelewa changamoto zinazowakabili, hasa katika vituo vya afya, hususan kwa wagonjwa wenye magonjwa sugu, wazee, vijana, na watoto wadogo. Huu uhusiano mzuri ulinisaidia sana wakati wa kukusanya data zangu.


Maendeleo Katika Kituo cha Afya Chalangwa

Kituo cha Afya Chalangwa, ambacho kilikuwa sehemu ya mradi wetu wa Kijana na Afya Bora, kinaendelea vizuri na kimepiga hatua kubwa ikilinganishwa na zamani. Huduma mpya kama vile meno na kinywa, upasuaji, na usafiri wa wagonjwa zimeongezeka, pamoja na ongezeko la majengo kama wodi za mama na mtoto. Pia, jamii imeonyesha mwamko mkubwa, hususan katika matumizi ya dawa za hospitali na idadi ya kina mama wanaojifungua hospitalini imeongezeka. Elimu kuhusu afya ya uzazi kwa vijana na chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano imeimarishwa.


Uwakilishi wa Changamoto za Jamii

Mradi wetu wa Kijana na Afya Bora ulifanyika vizuri, na kama Champion, nilipata nafasi ya kuwakilisha changamoto za jamii katika upatikanaji wa huduma za afya. Pia, niliweza kujua changamoto wanazokutana nazo watoa huduma, kama vile upungufu wa vifaa tiba na miundombinu wakati wa kutoa huduma.


Utekelezaji wa Mradi

Mradi wa Kijana na Afya Bora ulifanyika katika Kituo cha Afya Chalangwa, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, karibu na Chunya mjini. Tuliendesha mradi wetu kuanzia tarehe 17/4/2024 hadi 18/4/2024, na lengo kuu lilikuwa kusaidia jamii katika masuala ya afya, pamoja na kuisaidia serikali kutambua mapungufu yanayojitokeza kwenye utoaji wa elimu ya afya na kushirikisha jamii kwenye maamuzi.


Hitimisho

Kwa hitimisho, nilifanya kazi kwa kushirikiana na wenzangu, tukigawana majukumu ili kupata data kamili zilizohitajika. Tulipata msaada mkubwa kutoka kwa viongozi wetu waliotuongoza kwa ufanisi. Namshukuru kila mmoja aliyechangia katika safari hii, na pia kwa nafasi niliyopewa kama Champion ili kuwakilisha changamoto za jamii yangu na kuchangia maendeleo chanya. Shukrani zangu za dhati kwa wote walionifundisha na kunielekeza wakati wa mradi huu.

10 views0 comments

Comments


bottom of page